SPORTS

SPORTS

USAJILI LIGI KUU VODACOM MSIMU WA 2017/18

KATIBU Mkuu wa klabu ya soka ya Yanga, Charles Mkwasa, amesema hakuna mchezaji wao mwingine atakayesajiliwa na mahasimu wao Simba baada ya Haruna Niyonzima kufanya hivyo wiki mbili zilizopita.

Yanga ipo kwenye mapambano ya kuhakikisha inawabakiza nyota wake waliomaliza mikataba na wapinzani wao Simba, wamekuwa mstari wa mbele kuwarubuni nyota hao ili kujiunga na kikosi chao.

Akizungumza na gazeti hili, Mkwasa alisema mikakati iliyopo hivi sasa baada ya kumalizika kwa Mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani, ni kuwasainisha mikataba mipya wachezaji wao wote ambao wamemaliza mikataba yao na hiyo inatokana na kukamilika kwa mazungumzo na nyota hao.

“Ndani ya wiki hii, tunatarajia kumalizana na Thabani Kamusoko, Amisi Tambwe na wengine ambao wamemaliza mikataba yao na baada ya hapo tutakuwa na kikao na Vicent Bossou ambaye naye yupo kwenye mipango yetu ya msimu ujao,”alisema Mkwasa.

Katibu huyo alisema mambo yao yanakwenda kisomi zaidi na hawaoni haja ya kukurupuka kwenye vyombo vya habari na mitandaoni, kwa sababu timu yao ya usajili imejipanga vizuri na wanaelewa wanachokifanya.

Mkwasa alisema wanataka kujenga kikosi ambacho kitafanya maajabu kwa kufanya vizuri na kuvunja rekodi ya kufika mbali kwenye michuano ya Kimataifa na siyo kuwafunga watani zao Simba.

“Usajili tunaoufanya sisi Yanga, utalenga kucheza fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika na siyo kuwafunga Simba na ndiyo maana unaona tunafanya mambo yetu taratibu muda siyo mrefu ukimya wetu utatoa majibu yake na wale wanaotudharau watarudisha heshima,” alisema.

Aidha, Mkwasa amewataka mashabiki wa timu hiyo kuwa watulivu na kutoa nafasi kwa Kamati yao ya Usajili kufanya kazi yao ipasavyo ili mwisho wa siku waweze kufanikisha kile ambacho walikikusudia ambacho ni kuwapata wachezaji wote iliyokuwa imekusudia kuwasajili kwenye kipindi hiki cha usajili.

Mpaka sasa Yanga imesajili wachezaji watatu pekee ambao ni Abdallah Hajji ‘Ninja’, Ibrahim Ajibu na Pius Buswita kutoka Mbao FC ya Mwanza.