Kesi ya Kubenea, Makonda ya rindima Kisutu

Kesi ya Kubenea, Makonda ya rindima Kisutu
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (44) amekana kumtukana Mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda tarehe 14 Desemba 2015 walipokutana katika Kiwanda cha Tooku Garments Co. Ltd. kilichopo eneo la External Mabibo kwa madhumuni ya kutatua mgogoro kati ya wafanyakazi na uongozi wa kiwanda hicho
 
Katika kesi inayosikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Wakili wa Serikali mwandamizi, Kishenyi Mutalemwa alimsomea mshtakiwa maelezo ya kesi hiyo ambapo baadhi  ya mashtakiwa aliyakana.
 
Akisomewa maelezo ya kesi, Saed Kubenea alikiri kuwa ni mbunge wa Ubungo na pia alikiri kuwa anamfahamu mlalamikaji katika kesi hiyo kuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Makonda na kwamba ni kweli kuwa tarehe 14 Desemba 2015 alifika katika Kiwanda cha Tooku Garments Co. Ltd kulikokuwa na mgomo wa wafanyakazi.
 
Hata hivyo, alipoelezwa kuwa anashtakiwa kwa kosa la kumtolea lugha chafu Makonda ambapo alimwita kuwa ni kibaka, mpumbavu, mjinga na cheo chake ni cha kupewa kitendo ambacho kingeweza kusababisha uvunjifu wa amani na utulivu; Saed Kubenea alikana.
 
Kufuatia Kubenea kukana mashitaka yanayomkabili, Hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo , Thomas Simba alisema mashahidi sita wa upande wa mashtaka wataanza kutoa ushahidi wao Januari 20 na 21, 2016 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.